Dar es Salaam. Mtaalam wa Mawasiliano wa Shirika la kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) Tanzania, Usia Nkoma amewataka wahariri kutoka vyombo vya habari nchini wawe chachu kubwa ya kusimamia habari zitakazosaidia katika kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga nchini.

Akizungumza katika semina ya wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari iliyoratibiwa na Kampuni ya True Vision Production (TVP), kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na UNICEF, Nkoma amesema vyombo vya habari vina nguvu ya kuelimisha jamii, hivyo ni wakati muafaka vikaanza kuchukua hatua.

“Tutumie vyombo vyetu vya habari kuchochea habari zinazowahusu mama mjamzito na mtoto mchanga ili kupunguza vifo vyao visivyo vya lazima,”

“Kwa kufanya hivyo, tutawafanya watunga sera na watendaji wachukue hatua za haraka”, amesema Nkoma.

“Mbali na vyombo vya habari mnavyoviongoza, pia nawaomba mtumie akaunti zenu binafsi za mitandao ya jamii kuwa sehemu ya kampeni ya kuzuia vifo zinavyotokea hapa nchini,” ameongeza.

Mtaalamu wa Mawasiliano wa UNICEF Tanzania, Usia Nkoma akita made katika semina ya wahariri ya kusaidia kuokoa vifo vya mama wajawazito na watoto vinavyotokana na uzazi

SOMA ZAIDI:

Kwa mujibu wa takwimu, Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 duniani zinazoongoza katika vifo vya mama wajawazito na watoto vinavyotokana na changamoto mbalimbali za uzazi, zikiwemo kutokwa na damu nyingi wakati na baada ya kukifungua, ukosefu wa chanjo na umbali wa vituo vya afya katika baadhi ya maeneo.

Nchi nyingine ni India, Bangladesh, Nigeria, Jamhuri ya Watu wa Congo, Ethiopia, China na Palestina.

Amesema kutokana na takwimu kuonyesha vifo vipo juu, UNICEF Tanzania inashirikiana na wadau , ikiwemo serikali, taasisi na mashirika katika kuhakikisha mama na mtoto wanavuka salama katika kipindi cha uzazi.

Theophil Makunga, mmoja wa wahariri wakongwe nchini, akichangia katika semina ya wahariri yen lingo la kusaidia kupunguza vino via mama wajawazito na watot0 vinavyotokana na changamoto za uzazi

Akizungumza katika semina hiyo, mmoja wa wahariri na waandishi wakongwe, Theophil Makunga amesema takwimu za vifo vya mama wajawazito na watoto zinatisha, hivyo ni muhimu waandishi wakatumia kalamu zao kuhakikisha vifo hivyo havitokei.

“Kazi ya waandishi wa habari ni kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha, hivyo katika maeneo haya matatu, kuelimisha jamii ni kazi yetu,”

“Hivyo nadhani wajibu wa waandishi sio tu kuandika habari mbaya, bali pia wajibu kuandika habari zinazohusu maendeleo ya jamii na kutoa suluhisho la matatizo yanayojitokeza ili hatua zichukuliwe na jamii, watendaji na watunga sera,” amesema Makunga.

Bi. Pili Mtambalike akichangia mada katika semina ya wahariri ya kusaidia kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto vinavyotokana na uzazi

Pili Mtambalike, miongoni mwa waandishi wakongwe aliyewahi kushika nafasi mbalimbali katika Baraza la Habari Tanzania (MCT) amesema ana imani mtazamo wa vyombo vya habari katika kuandika habari zinazowahusu mama wajawazito na watoto utabadilika, baada ya semina hii.

“Siku zote, habari zinazohusu siasa, watu maarufu zimekuwa zikichukua nafasi sana katika vyombo vyetu vya habari, lakini, nina imani, semina hii itasidia kubadilisha fikra za wahariri wengi na kutoa kipaumbele pia katika habari zinazowahusu mama wajawazito na watoto katika maeneo yao ya kazi,” amesema Mtambalike.

TVP, kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na UNICEF, imeandaa semina tatu kwa kada tofauti katika kuhakikisha jamii inaelimishwa juu ya umuhimu wa kuwasaidia mama wajawazito na watoto wavuke salama.

Takwimu zinaonesha asilimia 50 ya watoto walio chini ya miaka 5 nchini Tanzania hufariki ndani ya mwezi mmoja baada ya kuzaliwa. Wanawake wajawazito 8,200 hufariki kwa mwaka wakati wakijifungua.

Moja ya malengo ya Kampeni ya ‘Jiongeze Tuwavushe Salama’ ni kupunguza vifo vya wanawake wajawazito, kutoka 556 mpaka 292, kama sio kumaliza kabisa ifikapo mwaka 2020.

Pia kampeni imeweka malengo ya kuokoa vifo vya watoto wachanga kutoka 43, mpaka 25 kwa vizazi hai 1,000 ifikapo mwakani.

Baada ya semina ya wahariri, kesho (23/04/2019) kutakuwa na semina itakayohusisha viongozi wa dini katika ukumbi wa hoteli ya Regency, iliyopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam. Semina ya mwisho itafanyika Ijumaa, ikiwahusisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini.

Kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama ni kampeni ya Taifa, iliyozinduliwa na Makamu wa Rais, mheshimiwa Samia Suluhu Hassan mjini Dodoma, mwezi Novemba mwaka jana, ukiwa ni mwongozo kutoka Wizara ya Afya kwa wakuu wote wa mikoa Tanzania Bara kuchukua hatua za kuzuia vifo vya mama na mtoto katika mikoa yao.

Madhumuni ya Serikali ni kuhamasisha viongozi wake, viongozi wa dini, mashirika yasiyo ya serikali, wadau wa maendeleo, watoa huduma za afya, familia na jamii kwa ujumla kuanza kuchukua hatua za kuzuia vifo hivyo.

Baadhi ya sehemu ya wahariri wakiwa katika semina.

KWA MAWASILIANO-BONYEZA HAPA