Na Mwandishi Wetu

Katika kuhakikisha mwaka 2020 unakuwa na mafanikio zaidi katika kazi zake, kampuni ya True Vision Production (TVP) imejiwekea mipango mikakati kabambe katika kuhakikisha inafanya kazi zake katika ufanisi na kwa mafanikio makubwa.

Kupitia mkutano wa kikao kazi uliofanyika katika Hoteli ya White Sands jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Kila idara ilipata nafasi ya kuangalia mafanikio na changamoto za kazi zilizofanyika mwaka jana na kazi ambazo bado zinaendelea (ongoing).

Lakini pia kikao hicho kilijadili kuhusu suala la ubunifu (kupitia kitengo cha creativity) katika kuhakikisha unafanyika ili kazi zinazozalishwa zizidi kuwa na ubora na mvuto kwa wateja na hadhira.

Wafanyakazi wa kampuni ya True Vision Production kwenye kikao cha pamoja kilichofanyika kwenye hoteli ya White Sands, Jijini Dar es salaam.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa TVP, David Sevuri aliwashukuru wafanyakazi kwa kuufanya mwaka 2019 kuwa wa mafanikio na kuahidi kuzidi kuweka mazingira mazuri zaidi kazini, ili kuongeza tija katika kazi zao.

“Teknolojia inazidi kukua na kuweka changamoto zaidi kwa wazalishaji wa vipindi/makala za telesheni, redioni na mtandaoni’

“Lakini katika kuhakikisha hatubaki nyuma tunaendana na kasi na mahitaji, TVP itaendelea kununua vifaa (equipments) vipya ili kuzidi kutoa kazi zenye ubora,” alisema Sevuri.

Mkurugenzi wa kampuni ya True Vision Production (TVP), David Sevuri akiongea na wafanyakazi wa kampuni hiyo wakati wa kikao cha pamoja kwenye hoteli ya White Sands Jijini Dar es salaam

Wafanyakazi kutoka idara tofauti, kama vile ubunifu, editing, Cameramen, sound & lighting, udereva, utafutaji masoko, uandishi wa script ( kwa ajili ya matangazo ya redio na televisheni) na wengine wengi ni miongoni mwa waliohudhuria kikao kazi, ambacho kilitoa pia fursa kwa wafanyakazi kuukaribisha mwaka mpya kwa michezo na burudani.

Mmoja wa wafanyakazi, Stephano Lihedule alisema kikao hicho kina umuhimu sana katika utendaji wa kazi katika kuhakikisha TVP inabaki kileleni katika kutoa kazi zenye ubora zaidi.

Lilian Revocatus alisema akiwa kama mmoja wa wafanyakazi anajivunia kufanya kazi katika kampuni ambayo imewekeza zaidi katika kukuza ubunifu kwa wafanyakazi na kampuni kupitia vifaa vinavyoenda na wakati na kuchagiza ubunifu.

Naye Sevuri amesema motisha itakuwa inatolewa kwa wafanyakazi ili wazidi kujituma na kubuni mikakati ya kuzalisha zaidi.

Wafanyakazi wa kampuni ya True Vision Production kwenye kikao cha pamoja kilichofanyika kwenye hoteli ya White Sands, Jijini Dar es salaam.

TVP imekuwa ikijizolea sifa ndani na nje ya nchi kwa kuzalisha Video zenye ubora wa hali ya juu. Ikumbukwe tu siku chache zilizopita TVP ilitunukiwa tuzo mbili za kimataifa za ITFF kutokana na Makala ya video bora ya Ngorongoro Conservation Area.