Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa kupambana na ukatili wa kijinsia nchini (TGNP), Lilian Liundi (katikati) akifurahi na wadau muhimu akiwemo mama Getrude Mongella (kulia), aliyekuwa Spika wa Bunge la Afrika

Ukatili wa kijinsia bado ni ajenda muhimu katika jamii ya Kitanzania, ndio maana True Vision Production (TVP) kwa kushirikiana na TGNP Mtandao imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha Tamasha la 14 la Jinsia linawafikia watu popote walipo duniani kwa kulirusha mubashara (live) katika mitandao ya kijamii kama vile You Tube, Facebook, Twitter na Instergram.

Katika kushiriki jitihada za kuhakikisha ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto wa kike unakomeshwa. Ni muhimu elimu ikatolewa kwa jamii na ndio sababu TGNP Tanzania ikaipa jukumu TVP la kutengeneza  video fupi zilizotokana na Tamasha. Lakini pia kufanya mahojiano na viongozi mbalimbali pamoja na kuandaaji chapisho maalumu  kwa lengo moja tu kuhakikisha tamasha hilo na meseji zilizotolewa zina ‘trend’ katika mitandao ya kijamii na kazi ilifanikiwa sana.

“Tangu tamasha lianzishwe mwaka 1996, zaidi ya watu 30,000 wamefikiwa katika kusimamia na kupaza sauti pale TGNP inapoona mambo hayaendi sawa,” alisema Lilian Liundi, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP.

Liundi alisema tamasha la mwaka huu (lililofanyika Septemba 24-28 mwaka huu) limekuwa na mafanikio, kikubwa zaidi likisherehekea miaka 25 ya TGNP, miaka 14 ya Tamasha lenyewe na miaka 25 ya azimio la mpango kazi wa Beijing uliokuwa la lengo la kupambana na ukatili wa kijinsia duniani.

Amesema TGNP inajivunia na harakati zinazoendelea juu ya kukomesha ukatili wa kijinsia katika kuhakikisha pamoja na mambo mengine, usawa unakuwepo kati ya wanawake na wanaume.

Ameongeza TGNP inafanya kazi na mashirika/taasisi mbalimbali vikiwemo vikundi vya haki za binadamu katika kuzikabili sera zinazokandamiza wanawake hasa katika nchi maskini.

 

Mama Getrude Mongella alikuwa mgeni rasmi katika tamasha la 14 la Jinsia na hapa akitoa neno lake mbele ya hadhira

Mama Getrude Mongella, spika wa zamani wa bunge la Afrika na aliyeongoza ajenda ya Beijing ya ukombozi wa mwanamke ameitaka TGNP kutengeneza machapisho yanayoelimisha ukatili wa kijinsia kwa kutumia fursa ya lugha ya Kiswahili kuteuliwa kuwa ndio lugha rasmi katika nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Naye spika wa zamani wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama Anna Makinda amewataka wanawake kugombania nafasi za uongozi katika chaguzi zijazo za serikali za mitaa na za ubunge.

“Wanawake ndio tunashiriki sana katika shughuli za kijamii kama vile misiba na sherehe, hivyo tunakubalika katika jamii na tuna nafasi ya kuwa viongozi, badala ya kutumika kuwapigia debe wengine” amesema Mama Makinda.

 

Naibu Waziri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Daktari Faustine Ndungulile akitoa neno kwa niaba ya serikali wakati wa tamasha la 14 la Jinsia

Akizungumza kwa niaba ya serikali, Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Dr. Faustine Ndungulile ameipogeza TGNP kwa kazi inayofanya, huku akisema serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha usawa wa kijinsia unakuwepo na kutatua changamoto kwa kuweka madawati ya kijinsia sehemu mbalimbali.

Amesema Tanzania inapambana na ukatili wa kijinsia na imekuwa mstari wa mbele wa kutoa fursa kwa wanawake mbalimbali. Akitoa mfano wa wanawake mbalimbali kushika nafasi kubwa za uongozi kama vile Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan.

Amesema kitendo cha serikali kutoa elimu bure ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha wasichana wanapata elimu, ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha kuja kuwa viongozi wa sehemu mbalimbali.

Ametoa wito kwa TGNP kuhamasisha wanawake kushiriki katika chaguzi zijazo badala ya kutegemea nafasi za kuteuliwa.

Waziri Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba alitoa neno wakati wa tamasha, akisema wanawake ni sehemu ya umoja wa taifa.

Naye Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba amesema wanawake wamekuwa sehemu ya kulinda umoja wa taifa la Tanzania na walikuwa na dhana hiyo walipotoa maoni yao katika mapendekezo ya rasimu ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema itafika wakati mfumo wa asilimia 50/50 kati ya wanawake na wanaume utakuwa haukwepeki.

Balozi wa Sweden nchini Tanzania Anders Sjoberg alisema wanaongeza nguvu katika mahusiano yao na serikali, TGNP katika kupambana na ukatili wa kijinsia nchini Tanzania

Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Anders Sjoberg amesema dunia inahitaji mabadiliko, pasipo usawa wa kijinsia, hakuna demokrasia.

Amesema usawa wa kijinsia ni ajenda pia ya nchi yake. Huku akiipongeza serikali ya Tanzania, TGNP na wadau wengine katika kuhakikisha ajenda hiyo inafanikiwa.