Binadamu amepewa kipaji na maarifa na Mwenyezi Mungu. Lakini uwezo/maarifa yake huenda yasionekane endapo hatopewa nafasi na watu wanaomzunguka katika jamii.

Kupitia binadamu sisi wenyewe, Mungu anaonesha maarifa/vipaji tulivyonavyo.

Ndio maana, Constantino Maro anasema kampuni ya True Vision Production (TVP), inayojihusisha na utengenezaji wa Makala za video, vipindi vya redio na uandikaji maalumu wa makala za magazeti, ndio imempika na kupikika kitaaluma. Na leo hii, Azam TV, ikiwa ndio mwajiri wake, ina mwamini katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji wa video (video production), ikiwemo kuhariri (editing), switching (kuchanganya picha),  mpiga picha ( camera operator ) na muongozaji (director) katika matukio mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.

Constantino Maro akiwa katika majukumu yake nje ya nchi.

Kifupi, yeye ni kama studio inayotembea ikiwa imekamilika

“TVP imenifundisha kazi kwa zaidi ya miaka 6 niliyofanya  toka nilipojiunga mwaka 2008, nikiwa kama mhariri wa video (editor). Na baadae nikajifunza vitu vingi sana na kuwafundisha wengi waliokuja kabla ya mimi kuondoka mwaka 2014,” anasema Maro.

Kikubwa zaidi anasema amejifunza kufanya kazi kwa bidii na kujituma mwenyewe katika muda wa ziada wa kazi, akiwa chini ya mkurugenzi wa TVP, David Sevuri.

David Sevuri,  Mkurugenzi wa TVP

“Sevuri ndio mtu ninayemhusudu kikazi (role model) wangu katika kazi za kuandaa na kutengeneza program za video na maisha yangu kwa ujumla.

“Wakati natoka TVP mwaka 2014, nilimwambia nitakuwa balozi mzuri wa TVP, ndio maana mafanikio ya kikazi ninayoyapata leo pale Azam yanatokana na TVP”.

Constantino Maro  na team ya TVP wakiwa kazini wakati huo kabla ya kuhamia sehemu mbalimbali na baadae Azam, anakofanya kazi hivi sasa.

“TVP haikuwa ni ofisi tu katika maisha yangu , bali ilikuwa ni chuo pia, unakwenda kazini (field) ukiwa na watu wenye uzoefu na wanakufundisha kazi, ukijiongeza kujifunza chochote kinachohusu video na utengenezaji sauti (audio) utaweza”

“Leo hii pale Azam nafanya kazi ya maeneo mbalimbali ya uzalishaji wa vipindi vya televisheni, nikiwa kama mpiga picha (video shooter) na mhariri pia (editor), miongoni mwa vile ninavyovifanya.”

“Nimeweza kwenda Kenya kufanya kazi katika uchaguzi wao mkuu wa mwaka 2016 na ule wa marudio, nikiwa kama mhariri na kuongoza matukio yote ya moja kwa moja (live),”anasema Maro.

Constantino Maro akiwa katika majukumu yake ndani ya studio za Azam TV

“Pia nimeweza kufanya miongoni mwa kazi nyingine kubwa kama vile kuwa muongozaji (director) wa shughuli ya mchakato mzima wa kumpata mgombea wa Uraisi wa mwaka 2015 kupitia Chama Cha Mapinduzi, hadi alipopatikana mgombea wake, Daktari John Pombe Magufuli na kuapishwa kwake akiwa kama Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sherehe zilizofanyika katika uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Pia nilifanya kazi ya uchaguzi mkuu wa Raisi kupitia slogan (kauli mbiu)  ya Azam inayosema ‘Azam TV, Kituo Cha Cha Uchaguzi ,” anasema Maro.

Kazi nyingine kubwa aliyoifanya ni kuwa muongozaji wa tamasha la filamu la Sinema Zetu (SZIFF), ukiachia ile ya kuwa muongozaji/switcher wa matukio ya moja kwa moja (mubashara) ya mechi za mpira wa miguu (ligi kuu Tanzania Bara), mechi za kimataifa na yale matukio mengine ya kitaifa na ya kimataifa, kazi ambayo ni adimu kwa Tanzania, baada ya yeye kufanyiwa mafunzo ya kuongoza matukio ya Azam na wataalamu kutoka nchini Afrika ya Kusini.

ALIJIUNGAJE NA TVP?

Maro, kabla ya kujiunga na kampuni ya True Vision Production,  pia aliwahi kufanya kazi sehemu mbalimbali zinazojihusisha na video production kama vile Hot Media.

Mwaka 2006 aliwahi kufanya kazi APT-Chuo cha Uhasibu kitengo cha Video Production na baada ya mihangaiko kadhaa alikwenda nchini Uganda kabla ya kurejea.

Alijiunga na TVP mwaka 2008, ofisi zikiwa nyuma ya Chuo Cha Kodi (ofisi za sasa zipo Mikocheni kwa Mwinyi) na baada ya hapo, alijiunga na kampuni ya Hakneel Production, kabla ya kwenda kujiunga na kampuni ya Azam Media mwaka 2014, akiwa kama mkuu wa wahariri, kazi anayoifanya mpaka sasa.

Maro pia mara kadhaa, anasafiri nje ya nchi na kuwa mhariri na mpiga picha katika matukio makubwa kama vile Kombe La Dunia, lililofanyika mwaka jana nchini Russia kwa ajili ya watazamaji wa Azam TV na Watanzania kwa ujumla.

JE MARO ALIONDOKAJE TVP?

“Nilikuwa katika kipindi kigumu sana kuondoka TVP kwa sababu bosi wangu David Sevuri, alikataa mimi kuondoka, sio kwa sababu alikuwa hanitakii mafanikio, bali alikuwa bado ananihitaji na alitaka nijifunze zaidi kwa sababu nilikuwa na moyo huo,”

“Barua yangu niliikabidhi kwa aliyekuwa msaidizi wake, Grace Bitesigilwe Lymo (marehemu) lakini naye aliikalia na hakuikabidhi kwa Sevuri,akiamini huenda nikabadili mawazo yangu na kubakia TVP,” anasema Maro.

“Sevuri aliniongezea mshahara mara mbili, sambamba na wafanyakazi wengine, lakini, niliendelea kutamani kutoka ili nikapate changamoto zaidi sehemu nyingine,”

“Mwishoni alinikubalia na kuniambia naweza kurudi muda wowote endapo nitashindwa maisha ya kazi huko niendako,” anasema.

KINACHOMFANYA TVP IWE SEHEMU MUHIMU MAISHANI MWAKE

Maro anasema Sevuri hakuwahi kuwa bosi katika maisha yake ya kazi, bali alikuwa rafiki, aliyefanya naye kazi kwa ushauri na kutaniana naye muda unapopatikana nje ya mipaka ya kazi.

“Nilimuheshimu kama bosi wangu, lakini kikubwa zaidi kwake yeye ilikuwa ni kufanya kazi kwa bidii,”

“Tulifanya kazi  kwa bidi, hata baada ya masaa ya kazi,”

“Wakati mwingine kazi ya watu wengi ilifanywa na watu wachache kwa bidi na weledi wa hali ya juu. Ndio maana mpaka leo hii moyo huu wa kujituma bado ninao Azam,”

Kingine muhimu pia katika maisha yake ya kazi TVP, ni kufanikiwa kumpata mwenza wake wa maisha, Sophia Mgaza, ambaye, kila ofisi alipohamia, toka TVP, kwenda Haakneel mpaka Azam walihama pamoja, sehemu zote hizo, Mgaza akiwa bosi kwa mumewe.

TVP IMEMPATIA CONSTANTINO MARO MKE

Constantino Maro akiwa na mke wake, Sophia Mgaza

Watu wana sababu nyingi zinazowafanya wakutane na baadae kujenga mahusiano mema. Maro, mbali na kupata maarifa na ujuzi wa kazi TVP, pia alipata fursa za kukutana na mtu ambaye ni miongoni mwa wale muhimu sana maishani mwake. Kama asingefanya kazi TVP, si ajabu asingeweza kukutana na Sophia, lakini yote kwa yote, Maro anasema Mungu ana sababu kwa kila linalotokea maishani mwake. Alikutana na Sophia TVP wakiwa wafanyakazi wa kawaida, baadae wakajikuta mioyo yao inadunda pamoja, hivyo wakawa marafiki na hatimaye sasa hivi ni mama watoto wake.  Mahusiano yao ni ya kipekee,  kwa sababu yalianzia TVP, kwa pamoja wakahama na penzi lao kwenda Haakneel na sasa wanafanya kazi Azam. Wakiwa kazini wafanyakazi, wakitoka ni mume na mke.

Maro anasema Sophia ni mwanamke mwema kwake anayempa heshima na kwa pamoja, wakiwa kama marafiki wa karibu, wanajadili maendeleo na changamoto zao za kikazi na maisha kwa ujumla.

Licha ya mkewe kuwa ni bosi wake kikazi pale Azam, Maro anasema wakiwa nyumbani, wanakuwa mke na mume, lakini wakiingia tu geti la kazini, wanabaki kuwa wafanyakazi wa kawaida.

Constantino Maro akiwa na mke wake Sophia Mgaza pamoja na watoto wao.