Vipindi vya Azam TV ni vizuri, vinaelimisha na kuburudisha, lakini hakuna kinachotokea bila ya kuwa na mtu nyuma yake. Nyuma ya vipindi vyote vinavyozalishwa Azam TV, yupo Sophia Mgaza, akiwa kama mkuu wa Vipindi Azam, Mgaza ndio msimamizi wa uzalishaji wa vipindi mbalimbali vinavyorushwa na Channel mbalimbali, akihakikisha maudhui yote na sera za kampuni zinazingatiwa,ikiwemo kuzingatia vipindi vyenye tija na maadili kwa Watanzania.

Anasema mafanikio yake ya uongozi yanatokana na ufanyajikazi  kwa tija na kushirikiana vizuri na watu anaofanya nao kazi ili kwa pamoja kama ‘timu ya ushindi’ kuzalisha vipindi vizuri na vyenye kuvutia.

Mgaza anasema mwanamke ni kama mwanaume na ana uwezo wa kufanya kazi yoyote mahali popote.
Mgaza ni miongoni mwa wanawake wengi wenye kuamini wanawake wanaweza kuwa viongozi wazuri maeneo yao ya kazi na kuaminiwa, sio tu kwa sababu wakipewa nafasi, bali uwezo wao wa kazi ndio unawaweka mahali walipo.

Anasema sehemu nyingi alizofanya kazi amekuwa kiongozi kwa sababu asilimia 95 ya uwezo wake wa kujifunza kuwa kiongozi amejifunza kutoka True Vision Production (TVP). Na sasa anaweza kufanya vitu vingi, kuanzia kuandaa script, kuongoza (directing), uzalishaji mpaka kuandaa ripoti, licha ya kuhariri na kufanya video production. Yeye pia ni kama studio inayotembea.

Mgaza alianza mbali katika taaluma yake, baada ya kumaliza elimu yake ya chuo kikuu, akisomea masuala ya kutengeneza uzalishaji wa video. Mwaka 2010 alikuwa akifanya kazi na kampuni inayojulikana kama FG Production, akifanya miongoni na shirika la Haki Elimu kama mtangazaji wa vipindi vyao vya Tafakari.

Baadae kampuni ya TVP ilishinda tenda ya kutengeneza vipindi vya Tafakari, hivyo walivutiwa na utangazaji wa Mgaza, lakini mgaza alikuwa akifanya kazi na FG Production. Hivyo TVP, walivutiwa na utendaji kazi wa Mgaza na kumuomba ahamie TVP na kuwa mtangazaji wa vipindi vya Haki Elimu vya Tafakari.

“Nilikutanishwa na David Sevuri na alinipa fursa, nami nikaitumia vizuri,” Nimeweza kusafiri sehemu mbalimbali kuzalisha vipindi vya Tafakari na vipindi vingine nikiwa na TVP kama mtangazaji na producer. Sevuri alijenga uaminifu kwangu na akanipa kazi nyingi sana baadae,” anasema Mgaza.

“Kampuni ya TVP, kama ilivyo Azam, iliniamini na kunipa nafasi za uongozi, uaminifu wangu na utendaji wangu kazi mzuri leo hii umenifanya nizidi kuaminika kila nilipo kikazi na kupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wafanyakazi wenzangu kwa sababu bila wao siwezi kuongoza,” anasema Mgaza.

“TVP imenifundisha kuwa na nidhamu kazini (commitments), kujituma, kuwa na subira (passion), mapenzi ya kazi na kuwa tayari kufanya kazi nje ya muda wa kazi,” anasema Mgaza.

David Sevuri, Mkurugenzi wa True Vision Production

Anasema mwanzoni, wakati Mkurugenzi wa TVP, David Sevuri anawapa kazi nyingi walikuwa wanamuona kama vile anawaonea, lakini sasa wanamuelewa kwa nini alikuwa anafanya hivyo na kwa faida ya yao.

Anasema kufanya kazi sana ndio kumewafanya watu wengi waliowahi kufanya kazi TVP wahishimike mahali walipo kwa sababu wanafanya kazi sana kwa kujituma ili kutimiza malengo yao ya kazi.

“Tuliishi TVP kama ndugu , kikubwa zaidi kila mfanyakazi alijua kijijini (alikozaliwa) mfanyakazi mwenzake, kwa sababu tukisafiri, tulikuwa na kawaida ya kwenda kusalimia wazee wake,”

“Mfano kama mfanyakazi nyumbani kwao ni Mbeya, basi ikitokea safari ya kikazi ya kwenda Mbeya, basi wafanyakazi waliokuwa katika hiyo safari wanakwenda kusalimia wazazi wake/familia yake,”

Sophia Mgaza akiwa na mume wake, Costantino Maro

“Hii imetufanya tuwe ndugu zaidi na kimenifanya mpaka leo hii TVP nipaone bado kama nyumbani,” anasema Mgaza.
Mgaza, kila alipofanya kazi mume wake naye alifanya. TVP walikuwa wote na walipokwenda Haakneel Production walikwenda wote, yeye (mke) akiwa kama Mkurugenzi Mkuu pia.

Anasema kuhama kwao ni sehemu ya kutaka kujifunza zaidi na kupata changamoto mpya.
Akiwa kama mkuu wa Vipindi Azam, Mgaza ndio msimamizi wa uzalishaji wa vipindi mbalimbali vinavyorushwa na Channel mbalimbali, akihakikisha maudhui yote na sera za kampuni zinazingatiwa,ikiwemo kuzingatia vipindi vyenye tija na maadili kwa Watanzania.

Lakini pia anajivunia kuratibu matukio mbalimbali makubwa, kama vile tamasha la kimataifa la ZIFF linalohusisha nchi mbalimbali.

Sophia Mgaza akiwa na mume wake Costantino Maro

JE ANAMZUNGUMZIAJE MAHUSIANO YAKE NA MUMEWE KAZINI?

“Kwa jinsi tulivyo kazini, inakuwa ni ngumu hata mfanyakazi mwingine kujua kama sisi ni mtu na mkewe, tunaheshimu kazi na kuheshimiana, ila tukitoka, ni zaidi ya mume na mke, ni marafiki tunaotegemeana, kama unavyoona mguu wa kulia unavyotegemeana na mguu wa kushoto kutembea,”anasema Mgaza.

USHAURI WAKE KWA VIONGOZI

“Tunapata nafasi za uongozi, inabidi kuzitumia vizuri na kuhakikisha walio chini wanapata nafasi pia ya kujifunza ili nao waje kuwa viongozi.
“Ukipata nafasi ya uongozi, usiwe sababu ya watu wengine kudidimia kitaaluma, bali wajivunie wewe kuwa kiongozi wao, kama Sevuri anavyojivunia kwa vijana wake tulivyo hivi sasa,” anasema Mgaza.