Kampuni ya True Vision Production (Video Production Company), kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na UNICEF Tanzania, iliandaa semina maalum ya siku tatu yenye lengo la kutoa elimu itakayopelekea kuhamasisha kushiriki katika kampeni maalumu ijulikanayo kama “Jiongeze, Tuwavushe Salama” yenye lengo la kupunguza vifo vya mama wajazito na watoto.

Semina hiyo iliyoanzia Jijini Dar es Salaam kwa siku tatu na baadaye Zanzibar. Ilishirikisha wadau mbalimbali wa afya na sekta nyingine wakiwemo wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari, waandishi, viongozi wa dini na wadau wengine wa maendeleo. Huku lengo la Serikali likiwa ni kuhamasisha viongozi wa kada zote kuanza kuchukua hatua za kuzuia vifo hivyo.

Agnes Mgaya, Kaimu Mratibu wa Huduma ya Afya kwa mama na Mtoto mkoa wa Dar es Salaam akitoa mada katika semina ya kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama mama wajawazito na watoto wachanga

Moja ya malengo ya Kampeni ya “Jiongeze, Tuwavushe salama” ni kupunguza vifo vya mama wajawazito, kutoka 556 mpaka 292, kama sio kumaliza kabisa ifikapo mwaka 2020. Na kuokoa vifo vya watoto wachanga kutoka 43, mpaka 25 kwa vizazi hai 1,000 ifikapo mwaka 2020.

Takwimu zinaonyesha Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 duniani zinazoongoza katika vifo vya mama wajawazito na watoto vinavyotokana na changamoto mbalimbali za uzazi, huku asilimia 50 ya watoto walio chini ya miaka 5 nchini Tanzania hufariki ndani ya mwezi mmoja baada ya kuzaliwa. Huku Wanawake wajawazito 8,200 hufariki kwa mwaka wakati wakijifungua

Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha Elimu ya Afya Zanzibar ya mwaka 2018, kwa upande wa Zanzibar, jumla ya wanawake 191 wanapoteza maisha kati ya vizazi hai 100,000, huku matarajio ya wizara ya Afya yakiwa vifo 110 kati ya vizazi hai 100,000.

Viongozi wa dini mbalimbali, wawakilishi wa UNICEF na Wizara Ya Afya wakiwa katika picha ya pamoja baada ya semina ya Jiongeze Tuwavushe Salama.

SOMA ZAIDI:

Haya ndio mambo 5 yaliyoibuliwa kwenye semina ya “Jiongeze, Tuwavushe salama”

  1. Umuhimu wa Vyombo habari katika sekta ya Afya.

Licha ya kuwa vyombo vya habari uhabarisha na kuburudisha, lakini moja ya muhimili wake mkuu ni kuelimisha. Kupitia semina ya Jiongeze, Tuwavushe salama, baadhi ya viongozi mbalimbali pamoja na wahariri wa vyombo vya habari walitoa rai kwa vyombo vya habari kujikita sana kwenye kuelemisha hususani kwenye suala hili linaloangamiza nguvu kazi ya Taifa.

Moja wa wazungumzaji wa mjadala huo ni pamoja na Mtaalam wa Mawasiliano wa Shirika la kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) Tanzania, Usia Nkoma, ambapo alisema kuwa vyombo vya habari vina nguvu ya kuelimisha jamii, hivyo ni wakati muafaka vikaanza kuchukua hatua.

“Tutumie vyombo vyetu vya habari kuchochea habari zinazowahusu mama mjamzito na mtoto mchanga ili kupunguza vifo vyao visivyo vya lazima, Kwa kufanya hivyo, tutawafanya watunga sera na watendaji wachukue hatua za haraka”, Amesema Nkoma.

Mtaalamu wa Mawasiliano wa UNICEF Tanzania, Usia Nkoma akita made katika semina ya wahariri ya kusaidia kuokoa vifo vya mama wajawazito na watoto vinavyotokana na uzazi

  1. Upatikanaji wa Lishe Bora

Upatikanaji wa lishe bora unatajwa kuwa na nafasi kubwa katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi pamoja na vifo vya watoto wachanga,

Mchungaji Christosiler Kalata Kanisa la Kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, usharika wa Mbezi Beach, hakusita kuweka bayana kwa jinsi upatikanaji wa Lishe bora unavyochangia kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto.

“Lishe bora ina nafasi kubwa katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga. Tuelimishe jamii juu ya umuhimu wa kula chakula bora, kwa wakati na kwa kiwango kinachohitajika.”-Alisema Mchungaji Christosiler Kalata.

Mchungaji Christosiler Kalata akichangia hoja latina semina ya Jiongeze Tuwavushe Salama. Yenye lengo la kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga vinavyotokana na uzazi

  1. Rushwa

Suala la Rushwa nalo halikuachwa nyuma. Licha ya sababu nyingi zilizotolewa na wadau mbalimbali suala la rushwa nalo lilipata nafasi ya kuzungumzwa kama chanzo kinachochangia vifo vya mama wajawazito na watoto.

Pia swala la rushwa katika huduma za afya lishughulikiwe. Rushwa inachangia kusababisha vifo vya akina mama wajawazito. Baadhi ya wauguzi wanatoa huduma stahiki kwa wagonjwa wanaotoa rushwa tu. Hii sio sawa.”-Aliongea Mwakilishi wa BAKWATA Sheikh Hamid Masoud Jongo.

  1. Utandawazi

Utandawazi ni neno lililoanza kutumika miaka ya 1990, likimaanisha kukifanya kitu kuwa katika kiwango cha kimataifa, na kukihamisha nje ya mipaka na kukifanya kuwa cha wazi na kikafanywa na watu wa aina yote duniani.

Hali hii unaonekana kuwa pia kichechezi cha vifo vya mama wajawazito na watoto kama alivyosema Mchungaji Christosiler Kalata.

“Mimba za utotoni zinachangiwa kwa kiwango kikubwa na maswala ya utandawazi. Zamani tendo la ndoa lilikua la kificho, sahivi linatumika kibiashara. Tutoe elimu kwamba pamoja na mambo ya kisasa kuna mila na desturi nzuri za kuiga.” Mch. Kalata aliongeza; “

  1. Ukosefu wa vituo vya afya, wahudumu wenye utaalamu na maadili pamoja na elimu ya afya ya uzazi

  • Ukosefu wa vituo vya Afya

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambazo zimekuwa zikipoteza mama wajawazito na watoto kutokana na matatizo yanayotokana na uzazi, Licha ya jitihada zinazofanywa na serikali na wadau wengine wa katika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya.

Licha ya Serikali kujitahidi kwa kiasi kikubwa katika kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kila sehemu. Bado changamoto zipo kwenye baadhi ya maeneo. Hivyo juhudi zilizochukuliwa zainapaswa kuendelezwa kiasi kikubwa

  • Ukosefu wa Wahudumu wataalam na wenye maadili.

Wawikilishi walitooa maoni yao pia kuhusiana na suala la wahudumu kutokuwa rafiki kwa mama wajawazito.

 “Kuna maoni kwamba baadhi ya watoa huduma wanakua na lugha mbaya kwa wagonjwa. Kuna umuhimu wa kushughulikia hili”-Alisema mwakilishi wa BAKWATA Sheikh Jongo

Sheikh Hamid Jongo wa msikiti wa Manyema kariakoo dar es salaam

  • Ukosefu wa Elimu ya Afya

Elimu inayozungumziwa ni elimu inayohusu suala zima la afya ya mama na mtoto kabla na baada ya kujifungua, ikiwemo muda wa kunyonyesha kwa mtoto ambao ulitajwa kuwa miezi 6.

Ukosefu wa elimu ya afya, kukosekana kwa huduma muhimu, kama vile ukosefu wa hospitali, dawa za kutibu binadamu na vifaa tiba katika baadhi ya maeneno ni miongoni mwa sababu za vifo vitokanavyo na uzazi.

Baadhi ya sehemu ya wahariri wakiwa katika semina.

Kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama ni kampeni ya Taifa, iliyozinduliwa na Makamu wa Rais, mheshimiwa Samia Suluhu Hassan mjini Dodoma, mwezi Novemba mwaka jana, ukiwa ni mwongozo kutoka Wizara ya Afya kwa wakuu wote wa mikoa Tanzania Bara kuchukua hatua za kuzuia vifo vya mama na mtoto katika mikoa yao.

TVP (A Video Production  Company) ndio waratibu wakuu wa semina hiyo ambayo ilishirikisha manguli wa sekta ya habari, wakiwemo Theophil Makunga, aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited na Abdalom Kibanda kutoka New Habari na akiwa kama mwenyekiti wa zamani wa jukwa la wahariri (TEF).

Lakini pia Wataalam wa Mawasiliano wa Shirika la kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) Tanzania, Usia Nkoma pamoja na Bi, Tahseen Alam