Kukua kwa kasi kwa teknolojia inatajawa kuongeza changamoto kubwa hasa kwa wazalishaji wa vipindi mbalimbali vya televisheni pamoja na redio. Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa kampuni ya True Vision Production (TVP) bwana David Sevuri alipokuwa akiongea na wafanyakazi wa kampuni hiyo kwenye mkutano maalumu uliofanyika kwenye hoteli ya White Sands jijini Dar es salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.

Bwana Sevuri, amesema wao kama True Vision hawatakubali kubaki nyuma na maendeleo haya ya teknolojia. Watahakikisha kama kampuni inaendana na kasi ya teknolojia ili kuweza kukidhi matakwa ya walaji.

“Teknolojia inazidi kukua na kuweka changamoto zaidi kwa wazalishaji wa vipindi/makala za telesheni, redioni na mtandaoni’

“Lakini katika kuhakikisha hatubaki nyuma tunaendana na kasi na mahitaji. TVP itaendelea kununua vifaa (equipments) vipya ili kuzidi kutoa kazi zenye ubora,” alisema Sevuri.

Kwa upande mwingine licha ya kuwashukuru wafanyakazi kwa kuufanya mwaka 2019 kuwa wa mafanikio. Bwana Sevuri amezungumzia suala la motisha kwa wafanyakazi hao ikiwa kama chachu ya kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Sevuri amesema motisha itatolewa kwa wafanyakazi ili waendelee kujituma.

Ikumbukwe tu siku chache zilizopita kampuni ya True Vision Production ilitangazwa kuwa mshindi wa Tuzo mbili za kimataifa za ITFF za nchini Afrika Kusini kupitia video bora ya uhifadhi ya Ngorongoro Conservation Area.

True Vision imefanya kikao chake mwishoni mwa wiki iliyopita ikiwa ni katika kuhakikisha mwaka 2020 unakuwa na mafanikio zaidi katika kazi zake pamoja na kuweka mipango mikakati ili kuhakikisha inafanya kazi zake katika ufanisi na kwa mafanikio makubwa.