Semina ya kampeni ya ‘ Jiongeze Tuwavushe Salama ‘ imevuka bahari mpaka visiwani Zanzibar. Hii ni baada ya kufanyika kwa semina nyingine tatu hivi karibuni Tanzania Bara, zikihusisha washiriki kutoka makundi matatu, waandishi wa habari, wahariri na viongozi wa dini tofauti.

Baadhi ya waandaaji wa semina ya JIONGEZE kutoka kampuni ya True Vision Production (TVP)

Tayari timu ya waandaaji wa semina hii kutoka kampuni ya True Vision Production (TVP) imewasili visiwani Zanzibar kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya semina hii.

True Vision Production ni waratibu wa semina hizi kwa kushirikiana na UNICEF pamoja na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. TVP imepewa jukumu la  kuandaa makala maalumu za video (documentary), kuhakikisha kampeni hi, ambayo mlezi wake ni mheshimiwa Makamu wa Raisi Mama Samia Suluhu Hassan, inafikiwa na jamii kupitia mitandao ya kijamii (Facebook, YouTube, Twitter) na vyombo vingine vya habari, radio, televisheni na magazeti kwa kuandika habari na makala maalumu ili kuhamasisha jamii ishiriki kutokomeza vifo vya mama wajawazito na watoto.

Wataalam wa mawasiliano kutoka UNICEF, Tahseen Alam na Usia Nkoma

Wataalam wa mawasiliano kutoka UNICEF, Tahseen Alam na Usia Nkoma kwa kushirikiana na maofisa wa Wizara wa Afya wa Zanzibar ni miongoni mwa wanaotegemewa kuwa wawezeshaji wa semina hii ya siku moja.

Lilian Revocatus Msika, mratibu wa semina JIONGEZE

Lilian Revocatus Msika, mratibu wa semina hizi kutoka True vision production amesema  hii kwa viongozi wa dini hapa visiwani Zanzibar ni sehemu ya semina tatu kama hii zilizofanyika Tanzania Bara hivi karibuni kwa lengo la kuwahamasisha washiriki kuwa sehemu ya kampeni ya kupunguza vifo kwa mama wajawazito na watoto.

Kampeni ya ‘Jiongeze Tuwavushe Salama ni kampeni ya kitaifa, iliyozinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mheshimiwa mama Samia Suluhu Hassan mjini Dodoma, mwezi Novemba mwaka jana, ukiwa ni mwongozo kutoka Wizara ya Afya kwa wakuu wote wa mikoa kuchukua hatua za kuzuia vifo vya mama na mtoto katika mikoa yao.

Madhumuni ya Serikali ni kuhamasisha viongozi wake, viongozi wa dini, mashirika yasiyo ya serikali, wadau wa maendeleo, watoa huduma za afya, familia na jamii kwa ujumla kuanza kuchukua hatua za kuzuia vifo hivyo.

Kwa maelezo zaidi bonyeza hapa