Sekta ya kilimo ni moja ya sekta muhimu na ya kipaumbele iliyo kwenye mpango wa matokeo makubwa sasa (Big Result Now). Mpango huu wa BRN ulianzishwa mwaka 2013 chini ya ofisi ya Rais kwa madhumuni ya kuleta mabadiliko, motisha na nidhamu mpya katika kutekeleza miradi ya kipaumbele, ili kuweza kufikia malengo ya dira ya Taifa ya mwaka 2025.

Kilimo ndio sekta inayobeba sekta nyingine mbalimbali za kiuchumi. Sekta kama ya Viwanda inategemea sekta ya kilimo kwa asilimia kubwa sana. Hii ni kwa ajili ya kupata mali ghafi ambazo zinaweza kuzalisha bidhaa nyingine kwa mahitaji ya kila siku. Hivyo basi sekta hii inahitaji uangalizi mkubwa sana.

Kwa kuzingatia umuhimu wa sekta hii ya kilimo, shirika la Care International pamoja na WWF, waliamua kuzunguka kwa wakulima mbalimbali kwa ajili ya kutoa mafunzo juu ya kilimo bora (kilimo uhifadhi).

Kupitia wakulima kutoka kwenye Vijiji mbalimbali, CARE-WWF wametoa mafunzo kwa wakulima ya jinsi ya kuanzisha kilimo chenye manufaa. Si tu kilimo cha kutunza mazingira pekaa bali kilimo kinachoweza kuwaongezea mazao yao mara dufu. Hii ni pamoja na kuwatoa wakulima kutoka kwenye kilimo holela na kuhamia kwenye kilimo hifadhi.

Wakulima ambao wamepokea mafunzo hasa kutoka kwenye kijiji cha Majonanga, Nachingwea wamekiri kuona mabadiliko makubwa katika shughuli zao za kilimo. Mabadiliko hayo ni pamoja na upatikanaji wa mazao ya kutosha kwa ajili ya kuwaingizia kipato. Pamoja na chakula lakini pia kuweza kuhifadhi misitu yao tofauti na ilivyokuwa mwanzoni.

True Vision Production iliambatana na timu ya CARE-WWF kutembelea vijiji hivyo kwa ajili ya kuandaa vipindi maalumu pamoja na Makala kuhusiana na program za kilimo hifadhi zinavyowakomboa wakulima.

Mafunzo haya kama yanaendelea kuwa endelevu kwa wakulima yanaweza kuwa na tija katika sekta ya kilimo. Hii itasaidia kukuza uchumi wa Taifa na kuweza kufikia malengo ya dira ya Taifa yam waka 2025.