Zanzibar. Suala la umbali wa vituo vya afya, ukosefu wa wahudumu wenye utaalamu wa  kuzalisha pamoja na ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi vinatajwa kuwa ndio chanzo cha kuongezeka mara dufu kwa vifo vitokanavyo na uzazi Zanzibar,  ikiwa ni nje ya mategemeo ya vifo vilivyotegemewa kutokea.

Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha Elimu ya Afya Zanzibar ya mwaka 2018, wanawake 191 wanapoteza maisha kati ya vizazi hai 100,000, huku matarajio ya wizara ya Afya yakiwa vifo 110 kati ya vizazi hai 100,000.

Abdulrahman Kwaza, Msaidizi wa Mkuu wa Kitengo Cha Elimu ya Afya Zanzibar

SOMA ZAIDI

Akizungumza kwenye semina maalumu ya ‘Jiongeze Tuwavushe Salama’ iliyoshirikisha viongozi wa dini wa Zanzibar chini ya usimamizi wa kampuni ya True Vision. Msaidizi wa Mkuu wa kitengo Cha Elimu ya Afya Zanzibar, Bwana Abdulrahman Kwaza, licha ya kukiri kuwa changamoto hizo za afya ndio zinzochangia idadi ya Vifo kuongezeka, lakini pia ametoa wito wa kuongezeka kwa ushiriki wa jamii katika afya ya uzazi.

Bwana Kwaza amesisitiza pia kuwepo na mipango kabambe ya kuimarisha huduma za kujifungua chini ya wataalamu wa afya. Pamoja na uboreshwaji wa vituo vya afya na kuweka msisitizo katika lishe ya mama akiwa mjamzito na ya mtoto baada ya kuzaliwa pamoja na mama kufuata kanuni za  kumnyonyesha mtoto wake miezi 6 tangu anapozaliwa, kwani maziwa ya mama yanavirutubisho tosha vya kumlinda mtoto.

Kwa upande mwingine, Mtaalamu wa mawasiliano kutoka UNICEF, Usia Nkoma amesema jamii kwa ujumla ina wajibu wa kuhakikisha mama mjamzito anakwenda kliniki na kujifungua katika kituo cha afya na anatakiwa awe chini ya uangalizi wa wataalam wa afya masaa 48 baada ya kujifungua.

Usia Nkoma Mtaalamu wa mawasiliano kutoka UNICEF tanzania.

Sheikh Fadhil Soraga, ambaye ni katibu wa Mufti wa Zanzibar. Amesema viongozi wa dini wana dhamana ya kuhakikisha wanaelimisha jamii juu ya umuhimu wa kuokoa vifo vitokanavyo na uzazi.

Amesema Qur-an, kitabu cha Waislam. Kina sisitiza juu ya afya ya uzazi, kikimtaka mama aliyejifungua kumnyonyesha mtoto wake miaka miwili iliyotimia ili awe na afya njema. Naye Farashuu Khamis Musa kutoka ofisi ya Mufti amewashukuru waandaaji wa semina, akisema wataleta chachu ya kuokoa vifo hivyo.“Viongozi wa dini wana wafuasi wengi, hivyo naamini watafanikiwa katika vita hii’, amesema Farashuu.

Sheikh Fadhil Soraga,  katibu wa Mufti wa Zanzibar kwenye Semina ya Jiongeze Tuwavushe Salama

Semina ya “Jiongeze, Tuwavushe salama” inaratibiwa na kampuni ya True Vision Production (TVP) kwa kushirikiana na UNICEF Tanzania na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ni sehemu ya mwendelezo wa semina nyingine tatu zilizofanyika Tanzania Bara hivi karibuni na kuhusisha pia viongozi wa dini tofauti, waandishi wa habari na wahariri.

Kwa ajili ya kupata maelezo zaidi kuhusiana na kamapeni hii ya Jiongeze, Tuwavushe salama na taarifa mbalimbali kuhusiana na True vision na jinsi ya kuendesha kampeni mbalimbali bonyeza HAPA.